LIGI YA VODACOM TANZANIA BARA HADI DESEMBA 29

LIGI Kuu Tanzania bara iliyosimama kupisha michuano ya Chalenji itaendelea mwishoni mwa mwezi huu kwa mechi za raundi ya 12 zitakazochezwa kati ya Desemba 29 na 31, mwaka huu na Januari Mosi mwakani.

Vilevile mechi 16 kati ya 152 zilizobaki za Ligi hiyo zitachezwa kuanzia saa 8:00 mchana.

Kwa mujibu wa kanuni ya 15 (45) ya Ligi Kuu, mchezo wowote wa Ligi Kuu unatakiwa kuchezwa kati ya saa 8:00 mchana na saa nne usiku.

Uamuzi huo umefanywa ili kuongeza mechi ambazo zitaonyeshwa moja kwa moja (live) na mdhamini wa matangazo, hatua ambayo itaisaidia bodi ya Ligi kufuatilia kwa karibu uchezeshaji wa waamuzi na pia kutoa nafasi kwa wadhamini wa Ligi pamoja na wa klabu kuonekana zaidi.

Hivyo mechi 102 kati ya 152 zitaonyeshwa moja kwa moja ikiwemo zile zitakazopigwa uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambazo kwa kawaida zinachezwa kuanzia saa 1:00 jioni.

Mechi za raundi ya 12 ni Desemba 29; Azam vs Stand United (saa 1:00 jioni), Desemba 30; Lipuli vs Tanzania Prisons (saa 8:00 mchana), Mtibwa Sugar vs Majimaji (saa 10 jioni), Ndanda vs Simba (saa 10 jioni), Desemba 31; Njombe Mji vs Singida United (saa 8 mchana), Mbao FC vs Yanga (saa 10 jioni), Januari 1; Mbeya City vs Kagera Sugar (saa 10 jioni) na Mwadui vs Ruvu Shooting (saa 10 jioni).

Baada ya raundi 12, Ligi Kuu ya Vodacom itapitisha mechi za Kombe la Mapinduzi na raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Azam Sport litakalochezwa kati ya januari 5 na 7, mwakani kabla ya kuingia raundi ya 13 itakayofanyika kati ya Januari 13 na 17, 2018.  

No comments