LWANDAMINA: NAWATEGEMEA TAMBWE, TASHISHIMBI MBIO ZA UBINGWA YANGA

MABINGWA  watetezi wa Ligi kuu Tanzania Bara, timu ya Yanga wanakamata nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi kwa alama mbili lakini haikuwa kazi rahisi kwao kufikia hapo.

Yanga kwa muda mrefu wamecheza bila wachezaji wake muhimu wakiwemo Amis Tambwe, Donald Ngoma, Thaban Kamusoko na baadae kiungo wake mkabaji Papy Kabamba Tshishimbi raia wa Kongo ambaye alipata majeraha.

Kocha wa kikosi hicho, George Lwandamina amesema kuwa kurejea kwa Tambwe na Tshishimbi kumefufua matumaini ya kutetea ubingwa sambamba na kampeni zake za kushiriki kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

“Tulikuwa na kikosi kichanga wakati tunashiriki mechi za Ligi, namba kubwa a wachezaji waliotoa mchango mzuri msimu uliopita hawakuwepo uwanjani lakini sasa inatia moyo kuona wameanza kurejea,” alisema Lwandamina.

“Ligi ni ngumu msimu huu na kucheza bila wachezaji wako muhimu inakuweka kwenye mazingira magumu ua kupata alama tatu hivyo nafurahia kurejea kwa Tambwe na Tshishimbi ambao watatusaidia katika mechi zilizosalia,” aliongeza kocha huyo.

“Tunahitaji kuwa na kikosi kipana, mbele yetu kuna michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Kombe la FA, Kombe la Mapinduzi, lakini pia tunahitaji kutetea ubingwa wa Ligi,” alimaliza.


Yanga ilicheza mechi ya kirafiki na timu ya Polisi na kutoka sare ya bila kufungana. Huo ulikuwa ni mchezo wa kujipima nguvu ambapo Lwandamina alikuwa akitesti wachezaji aliowasajili kama wanaweza kuingia kwenye mfumo wake.

No comments