MSUVA ADONDOSHA CHOZI KILLI STARS KUBORONGA CHALLENGE CUP

WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva anayechezea timu ya Difaa Hassan El – Jadida ya nchini Morocco, ameumizwa na kuboronga kwa kikosi cha timu ya Kilimanjaro Stars katika michuano ya CECAFA Challenge nchini Kenya.

Msuva amesema kwamba amesikitishwa na matokeo hayo mabovu kwani kwa kiasi kikubwa wachezaji wanaokuwa kwenye kikosi cha bara ndio huunda taifa Stars.

“Ukitazama kikosi cha Challenge tumekosekana mimi, Banda na Mbwana Samatta, lakini kwa kiasi kikubwa kikosi ndio kilekile kinachotegemewa na taifa,” alisema Msuva.

Hata hivyo, Msuva alisema kuwa wanajipanga upya baada ya matokeo hayo ya kusikitisha ambayo yameacha simanzi kwa Watanzania.

“Ni mambo ya kawaida kwenye soka, wakati mwingine hata timu kubwa zinapata matokeo ya kustaajabisha kabisa katika michuano, kinachotakiwa kufanywa sasa hivi ni kujipanga upya,” aliongeza.

Timu hiyo ilipata sare moja tu ya 0-0 na Libya na kufungwa mechi nyingine zote tatu za Kundi A Kombe la Challenge, hivyo kutolewa mapema kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi.  

No comments