NJOMBE MJI YASAJILI WAWILI KUTOKA RWANDA

TIMU ya Njombe Mji imekamilisha usajili wa wachezaji wawili kutoka Rwanda kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya ngwe ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania bara.

Kocha wa Njombe Mji FC, Mlage Kabange amewataja wachezaji hao kuwa ni Herelimana Lewi kutoka Mukura Victory na Etienne Ngladjo kutoka Suarise FC, zote za Rwanda.

Pamoja na wawili hao kutoka Ligi Kuu ya Rwanda, kabange amesema pia wamewasajili wachezaji wengine watatu kwa mkopo kutoka timu tofauti.

Wachezaji hao waliochukuliwa kwa mkopo ni Mohammed Titi kutoka Singida United, Nickson Kibabange na Muhsin Malima wote kutoka Mtibwa Sugar.

Baada ya mapumziko ya wiki tatu kupisha michuano ya CECAFA iliyofikia tamati Jumapili nchini Kenya, Njombe Mji itateremka tena dimbani Desemba 31 kumenyana na Singida United kwenye uwanja wa Sabasaba.

Kwa sasa Njombe Mji wanashika nafasi ya 15 katika Ligi Kuu ya timu 16, ikiwa na pointi 8 baada ya kucheza mechi 11.

No comments