RUVU SHOOTING YAVUTA VIFAA VITANO VIPYA DIRISHA DOGO

TIMU ya Ruvu Shooting ya Pwani imeimarisha kikosi chake kwa ajili ya hatua iliyobaki ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kusajili wachezaji watano wapya kwenye dirisha dogo.

Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema kwamba wameamua kusajili wachezaji hao watano ambao wote vijana ili kukiongezea nguvu kikosi katika duru ya lala salama ya Ligi Kuu.

Bwire amewataja wachezaji hao wapya waliosaini mikataba ya kuitumikia Ruvu Shooting kuwa ni beki Rajab Zahir Mohamed, viungo Hamis Saleh Maulid, Adam Ibrahim Abdallah na washambuliaji Gideon Brown Benson na Alinanuswe Martin mwaisemba.

“Wachezaji hao tayari wako kambini wakiendelea na mazoezi isipokuwa Zahir pekee ambaye ataripoti kambini muda wowote kuanzia sasa,” amesema Bwire.

"Baada ya Ligi Kuu kusimama kwa wiki tatu kupisha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA, Ruvu Shooting itashuka dimbani Desemba 31 kumenyana na wenyeji, Mwadui FC Uwanja wa Mwadui Complex, shinyanga."

No comments