SIMBA SC YAANZA KAMBI CHAPCHAP MAPINDUZI CUP

TIMU ya Simba leo imeanza kambi yake baada ya kutolewa kwa ratiba ya michuano ya Kombe la Mapinduzi huku pia wakikabiliwa na kibarua kizito cha kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ambao umekwenda Yanga kwa misimu mitatu mfululizo.

Ratiba ya michuano ya Kombe la Mapinduzi imetoka na Wekundu wa Msimbazi wamepangwa kufungua dimba dhidi ya wageni URA kutoka Uganda katika mchezo utakaopigwa Januari 2 katika uwanja wa Amaan Zanzibar.

Watani wao wa jadi, Yanga wao wanatarajia kuanza na JKU ya Zanzibar Januari 1 katika uwanja huohuo wa Amaan.

Timu ya Azam FC ambao ni mabingwa watetezi wao watafungua dimba na Jamhuri katika mchezo utakaofanyika katika uwanja wa Amaan pia Januari 2.

Kipyenga cha kwanza kitapulizwa Desemba 30 kwa kuzikutanisha timu za Zimamoto na Mlandege.

Kundi la Simba linahusisha timu za Azam FC, Jamhuri, Taifa ya Jang’ombe na URA ya Uganda, wakati Yanga imepangwa kundi B pamoja na JKU, Mlandege, Zimamoto na Shaba.

Mtanange wa kukata na shoka utazikutanisha timu za Simba na Azam FC Januari 6, ambao waliwafunga mwaka jana kwenye hatua ya fainali.

Simba itaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare na Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu bara uliochezwa katika uwanja wa Azam Complex.

No comments