USAJILI WA KISHINDO WAIREJESHEA MATUMAINI RUVU SHOOTING

KATIKA mechi 11 za Ligi Kuu Tanzania Bara walizocheza Ruvu Shootung SC ya Pwani wamejikusanyia jumla ya pointi 11 ambazo ni sawa na wastani wa alama moja kwa kila mchezo.

Wapo nafasi ya 13 lakini wametofautiana kwa alama nne tu na timu ya Stand United ambayo inakamata nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi.

Kelele za msemaji wao, Masau Bwire zilianza kupungua wakati wa mechi za mwishoni kabla ya kusimamishwa kwa Ligi hiyo kupitisha michuano ya Kombe la Chalenji nchini Kenya.

Msemaji huyo ameibuka tena na kunadi usajili uliofanywa ikiwa kama njia mojawapo ya kufanyia marekebisho kikosi chao kabla ya kuisha kwa mechi za mzunguko wa kwanza wa Ligi.

Ruvu Shooting iliingia sokoni kwa kasi na kunasa wachezaji watano ambao ni beki Rajab Zahir Mohamed, viungo Hamis Saleh Maulid, Adam Ibaim Abdallah na washambuliaji Gideon Brown Benson na Alinanuswe Martin Mwaisembe.

“Tunaelekea duru ya lala salama ndio maana tumeamua kusajili wachezaji hao watano na wote bado ni vijana wadogo, tunaamini wataweza kukiongeza nguvu kikosi chetu,” alisema Masau Bwire.

“Kikosi kipo kambini sambamba na wachezaji hao wote taliowasajili, ambae amekosekana ni Zahir lakini ataripoti muda wowote kuanzia sasa,”aliongeza.


Ruvu Shooting itacheza mechi ya kufungia mwaka Desemba 31 dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa Mwadui Complex, mkoani shinyanga.

No comments