AYA 15 ZA SAID MDOE: THAMANI YA USAJILI WA WANAMUZIKI WA DANSI IMESHUKA HADI SIFURI


Niliwahi kusema kuwa muziki wa dansi unapita kwenye miluzi mingi sana, miluzi ile ambayo tunaambiwa ikizidi humpoteza mbwa.

Kila mmoja anasema lake …wako wanaotaka dakika zipunguzwe (nyimbo ziwe fupi), wako wanaotaka magitaa yasipewe kipaumbele, wengine hawataki masebene achiliambali wale wanaotaka dansi iige kila kitu cha bongo fleva.

Lakini ukweli ni kwamba muziki wa dansi wala hauhitaji mageuzi makubwa, ni kiasi tu cha kuboresha tungo na kuacha kurefusha nyimbo bila sababu za msingi, kuachana na mtindo wa kutaja majina mengi ya wadau, jambo ambalo halina maana yoyote zaidi ya kuchafua tu nyimbo.

Wanaotakiwa kufanya mageuzi hayo ya msingi ni wanamuziki wenyewe wala sio wamiliki wa bendi, wadau wala mashabiki. Wadau wameshaongea mengi sana juu ya maboresho ya muziki wa dansi lakini wanamuziki wengi wamekuwa ‘viziwi’.

Majuzi nilibahatika kumsikia bosi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka, akiongea kupitia Clouds FM akisema kwamba nyimbo ndefu kama reli ya kwenda kwao Kigoma hazina nafasi tena ndani bendi yake, lakini pia alifafanua kuwa ni lazima wanamuziki wakubaliane na mahitaji ya soko la wakati uliopo kwa kutoa tungo bora na si bora tungo.

Asha Baraka akafichua pia kuwa kuna nyimbo nyingi za bendi hiyo zinaozea studio kwa vile tu hazikidhi vigezo na hivyo amezigomea kuingia sokoni.

Unaposikia kauli kama hiyo kutoka kwa mmiliki wa bendi unafarijika sana, unahisi kuwa angalau kuna harufu ya mapinduzi ya muziki wa dansi ingawa ni ukweli usio na chenga kuwa hatua hiyo imechelewa sana.

Ukipima kwa undani kauli ya Asha Baraka utabaini kuwa miongoni mwa watu wanaoudondosha muziki wa dansi ni wanamuziki wenyewe.

Wanamuziki wa dansi wamekuwa wavivu wa kufikiri, wazito wa kulipima soko, ma-mwinyi wa uwajibikaji, wachoyo, wabinafsi na waoga kufanya utafiti wa soko jipya la muziki wao.


Wanamuziki wa dansi wanashindwa kuongeza au kulinda thamani yao, wanajirahisi na hawakubali kufa na tai shingoni, hatua inayowafanya wengi wao wawe kiguu na njia kwenda kusaka show za ndondo za elfu kumi kumi.

Tatizo kubwa la wasanii wetu wengi ni shule ndogo na ni kama vile hawakutegemea kuwa hapo walipo, haikuwa ndoto waliyoisaka kwa udi na uvumba na ndio maana hawana muda wa kuyalinda mafanikio yao… wanaishia kuwa malimbukeni na mazumbukuku.

Kwa mfumo huo wa kulemaaa na show za ndondo, unategemea vipi thamani yako ya usajili ipande? Ni lini kichwa chako kitapata utulivu wa kutunga nyimbo nzuri wakati muda wote unawaza ndondo, umelemaa na nyimbo za kucopy.

Thamani ya wanamuziki wa dansi imeshuka na sasa hakuna tena mmiliki wa bendi anayeweza kumnunua mwanamuziki wa dansi kwa pesa ndefu, labda wadau na mashabiki wachangishane kumnunua msanii kwaajili ya bendi yao pendwa. Hata hivyo msanii atakayesajiliwa kwa nguvu za wadau basi kitu kinachoitwa mshahara atakisikia kwenye njozi.

Miezi mingi iliyopita niliwahi kuandika kuwa mmiliki anayemnunua mwanamuziki wa dansi kwa milioni 15 anahitaji kupimwa akili kwa vile hakuna namna yoyote ile ya mwanamuziki huyo kuongeza pato la bendi hadi kurejesha milioni 15 za ‘usajili’.

Wengi walinipinga sana na kuniambia nimeutukanisha muziki wa dansi, lakini leo tunaiona hali halisi, hakuna bendi inayoweza kumnunua msanii wa dansi hata laki moja na nusu achilia mbali milioni 15. Thamani ya usajili wa wanamuziki wa dansi imeshuka hadi sifuri.

-->

No comments