CHRISTIAN BELLA ATUA ZIGO LA UTEJA WA MADAWA YA KULEVYA …asema haishi maisha ya ‘oya oya’


Mwimbaji pekee wa muziki wa dansi aliyekataa show za kiingilio kinywaji, Christian Bella, amesema tuhuma zinazosambaa mitandano kuwa anatumia madawa ya kulevya, ni moja ya changamoto za kutengenezwa.

Bella amesema ziko mbinu za kurudishana nyuma zinazotengenezwa na baadhi ya watu kwa wasanii wenye mafanikio, lakini kamwe tuhuma za kutumia madawa ya kulevya haziwezi kumvunja moyo.

Akiongea na kipindi cha Weekend Bonanza cha Clouds FM Jumamosi usiku, Bella alikanusha juu ya matumizi ya madawa ya kulevya na kusema kwamba yuko tayari kwenda kupimwa mbele ya kamera za televisheni.

Katika onyesho lake la mkesha wa mwaka mpya ndani ya ukumbi wa Nefaland Hotel ulioko Manzese jijini Dar es Salaam, Bella alishindwa kutumbuiza na kulazimika kupelekwa hospital baada ya kuimba wimbo mmoja tu.

Bella akalazwa hospitali huku sababu kubwa ikiwa ni uchovu baada ya kufanya show nyingi mfululizo katika kipindi kifupi ndani na nje ya nchi.

Baada ya Bella kulazwa ndipo uzushi ukaanza kupitia mitandao ya kijamii kuwa mwimbaji huyo kazidiwa na matumizi ya madawa ya kulevya.

Katika maongezi yake na Clouds FM, Bella akatoa vyeti vya hospitali aliyolazwa ili kufafanua alichougua.

Bella amesema yeye haishi maisha ya ‘oya oya’ – maisha ya maskani na yale yenye fujo za matumizi ambayo mara nyingi ndio huleta vishawishi vya mambo yasiyofaa.

“Nimekuja Tanzania kufanya kazi, nipo hapa kwa mwaka wa 12 sasa, nimefanikiwa kujenga jina kubwa na kupendwa na Watanzania wengi, wanaojaribu kunichafua hawatafanikiwa,” alisemaa Bella.

No comments