DAH! ALLY CHOCKY NDIYO BASI TENA TWANGA PEPETA


Wakati Ally Chocky akisema mkataba wake ndani ya Twanga Pepeta unaisha mwenzi Machi mwaka huu na kwamba baada ya hapo atahitaji kuwa msanii wa kujitegemea, bosi wake Asha Baraka naye amefichua kuwa tayari wameanza maisha mapya bila Chocky.

Ally Chocky ameiambia Saluti5 kuwa utumishi wake ndani ya Twanga Pepeta unakoma rasmi miezi miwili ijayo, lakini tayari amekubaliana na uongozi wa bendi hiyo kuchomoka mapema zaidi.

Chocky amesema ameruhusiwa na Twanga kufanya mambo yake binafsi katika kipindi hiki cha kuelekea ukingoni mwa mkataba wake na hivyo atakuwa akionekana jukwaani kwa nadra.

“Katika kipindi ambacho sitaki kuachana vibaya na Twanga Pepeta basi ni kipindi hiki. Sitaki tena yale mambo ya kuapizana kutozikana.

“Namalizana na Twanga kwa amani kabisa na hata mkataba wangu utakapoisha, bado nitakuwa nikiitembelea kadri nafasi itakavyoruhusu,” alisema Chocky katika mazungumzo yake na Saluti5.

Lakini Asha Baraka naye katika mazunguzo yake na Weekend Bonanza ya Clouds FM, akasema mashabiki wa Twanga wasiulize tena kuhusu Ally Chocky kutoonekana jukwaani.

“Chocky mkataba wake unaisha mwezi wa tatu na tumemruhusu aanze kujiandaa na maisha mapya, hivyo mashabiki wasishangae sana kutomuona jukwaani.

“Tunajipanga safu mpya yenye watu wachache, hawa wasanii wenye majina makubwa ni vizuri tukawapa nafasi ya kwenda kufanya mambo yao binafsi,” Asha Baraka akaiambia Clouds FM.

No comments