IBRAHIM KANDAYA AFICHUA “NOTI YA ELFU TANO ILINIPONZA KUACHANA NA TAARAB”

MKUNG’UTAJI mahiri wa gitaa la Bass, Ibrahim Kandaya “Profesa” amefanya mazungumzo na Saluti5 na kufunguka kuwa, alianza sanaa kama mcheza sarakasi kwenye vikundi mbalimbali vya sanaa za maonyesho, kabla ya mwanzoni mwa miaka ya 90 kuangukia kwenye bendi ya Muungano Culture Troupe kama mcharazaji Drums.

Zaidi ya hilo, Kandaya anasema kuwa, kati ya miaka ya 1994 na 95 alijikuta tena akiipa kisogo fani ya mipasho na kutumbukia kwenye dansi akiponzwa na ujira wa sh.  5,000 aliopewa na bendi ya Zaita Muzika aliyokwenda kuisaidia siku moja baada ya wapigaji Drums wao kuchelewa kufika ukumbini.

“Siku hiyo sisi (Muungano) tulikuwa tunapiga Vijana Hostel na wao (Zaita Muzika) walikuwa Mango Garden na nilipotonywa kuwa wana pengo la mpiga Drums kwa siku hiyo nilitoroka kwenda kuwasaidia lakini ujira wa sh. 5,000 walionipa baada ya shoo ilinivutia zaidi na kunitia tamaa,” anasema Kandaya.

Kandaya anasema, aliporejea Muungano alikuta stori zimevuja kiasi cha kumfikia bosi wa Muungano, Norbert Chenga ambaye alimsimamisha kwa utovu huo wa nidhamu naye kuona kuwa ni bora aachane kabisa na taarab na kugeukia dansi moja kwa moja.

No comments