KOMANDOO HAMZA KALALA ARUSHA DONGO KWA WANAMUZIKI WA SASA

MKONGWE wa muziki wa dansi, Komandoo Hamza Kalala amesema kuwa anashangaa kuona kuwa wanamuziki wa siku hizi wamekuwa wavivu kutunga nyimbo za kusindikiza matukio muhimu ya kila mwaka zikiwemo sikukuu.

“Nafikiri ni uvivu tu wa wanamuziki wetu wa zama hizi, nakumbuka huko nyuma ilikuwa balaa, kipindi cha karibu na sikukuu kama vile Sabasaba, Krismasi na mwaka mpya watu walikuwa wanumiza vichwa,” amesema Kalala.

“Kila mmoja alikuwa anataka kuonyesha ufundi wake katika tungo zinazohusiana na matukio hayo, lakini hali hiyo imekuwa tofauti na sasa,” aliongeza mkongwe huyo.

Amesema kuwa, katika kipindi cha nyuma, hata ilipotokea taifa kukumbwa na maafa yakiwemo baa la njaa, mafuriko na ajali nyingine, wanamuziki walikuwa wepesi kuibuka na tungo za kufariji.


“Wasanii wabadilike, watuonyeshe umahiri wao katika tungo za namna hiyo sio kila siku kusikiliza vilio na sifa za mapenzi tu peke yake,” alimaliza Kalala aliyewahu kutamba na bendi za UDA Jazz, Vijana Jazz, Washirika na Bantu Group.

No comments