MWAKYEMBE ATOA SALAMU ZA POLE KWA MSIBA WA LIMONGA JUSTINE… watoto wake kulipiwa ada na vifaa vya shule, Radio Uhuru yasema pengo lake ni kubwa

WAZIRI wa Habari Utamaduni na Michezo, Dk. Harryson Mwakyembe ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu Limonga Justine aliyejiwekea jina kubwa kwa jamii na amewaomba wafiwa kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha simanzi na majonzi.

Amesema, anatambua ukubwa wa msiba huu hasa katika nyanja ya habari, lakini hata hivyo hakuna budi kuwa na uvumilivu na kumuombea Mungu marehemu apokelewe mahala pema. 

Naye bosi wa Nduvini Auto Garage ya jijini Dar es Salaam, Alhaji Ahmed Msangi ameonyesha kuguswa na tukio la msiba wa aliyekuwa mtangazaji wa Uhuru Fm, Limonga Justine aliyemwelezea kuwa ni miongoni mwa wanahabari waliotoa mwongozo wa kuigwa kwenye jamii.

Msangi amesema kuwa, alimfahamu vyema Limonga na kwamba alipopokea taarifa za kifo chake alihisi kuishiwa nguvu kutokana na ukaribu waliokuwa nao.

Bosi huyo ameahidi kuwa katika kipindi hiki cha kufunguliwa kwa shule, kampuni yake itawanunulia watoto wa marehemu vifaa vya shule zikiwemo sare pamoja na kuwalipia karo wakati wakisubiri kukaa na familia kuona namna ya kuwazesha watoto hao kielimu.

Wakati huohuo, kaimu mkurugenzi wa Uhuru Fm, Angel Akilimali amesema kifo cha Limonga aliyekuwa mwajiriwa wao kimeacha pengo kubwa ambalo halitazibika kirahisi.

Alisema Limonga alikuwa mhariri mbunifu aliyeweza kuongoza vipindi mbalimbali ambavyo vilipendwa na wasikilizaji wao. Angel ameahidi kuwa, stahiki zote za marehemu kama mwajiriwa zitapatikana kwa wakati.

Limonga amefariki dunia Desemba 30, mwaka jana katika hospitali ya TMJ alikolazwa akitibiwa. Ameacha mjane na watoto wawili ambapo mazishi yake yamefanyika leo katika makaburi ya Saku, Mbagala Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

No comments