SHOMARY ALLY WA VIJANA JAZZ AFICHUA SIRI YA WIMBO "USHINDE MOYO WAKO"


MCHARAZAJI mahiri wa gitaa la Solo kutoka Vijana Jazz Band, Shomary Ally ameweka wazi kuwa yeye ndie mtuzi wa wimbo “Ushinde Moyo Wako” wa Juwata Jazz Band “Msondo Ngoma” na si Isaya Swahiba kama wengi wanavyodhani.

Shomary amepiga stori na Saluti5 na kutonya kuwa aliutunga wimbo huo mwaka 1987 wakati akiwa Mwenge Jazz Paselepa na kilichotokea ni kwamba Isaya Swahiba aliyekuwa nae pamoja (Mwenge Jazz) aliupenda akauomba na kumpa.

“Mwaka mmoja baadae Swahiba alihamia Msondo na kwenda kuurekodia huko wimbo huo mwaka 1989,” amesema Shomary akisisitiza kuwa alimpa kiroho safi kwa kuwa walikuwa marafiki wa kutupwa.

Wimbo “Ushinde Moyo Wako” unapatikana kwenye albamu ya “Cheusi Magala” inayokusanya vibao vinane baadhi yake vingine vikiwa ni "Mizimu", “Missi”, “Usia wa Baba”, “Kambarage Nyerere”, "Tulipotoka ni Mbali" na “Ole Wasumbuka”.

Walioshiriki kuurekodi wimbo huo ni Abdul Ridhiwan “Pangamawe” kwa upande wa gitaa la Solo, Maneno Uvuruge (Rhythm) na Beka Semhando (Bass), wakati kwenye Drum Mabruki Halfan alisimama imara huku Buyungwa akiwa kwenye Tumba.


Ala za upepo katika wimbo huo zimepulizwa na Mnenge Ramadhani, Zito Mbunda, Roman Mng’ande “Romario”, Joseph Lusungu na Abdi Mketema huku waimbaji wakiwa ni mwenyewe, Swahiba, Tx Moshi William, Joseph Maina na Othman Momba ambao wote ni marehemu kwa sasa.

Pata nafasi ya kuusikiliza wimbo huo.

No comments