ZAHIR ALLY ZORRO AIPA USHAURI WA BURE SERIKALI... ataka eneo la Jangwani ligeuzwe "City Park"

MVUA ndogondogo zinazoendelea kumwagika jijini Dar es Salaam hivi sasa zimeonekana kumtisha mkongwe wa muziki Bongo, Zahir Ally Zorro ambaye amekuja na wazo binafsi kwa serikali ya Tanzania.

Zorro ameiomba serikali akiwa raia mwandamizi, kuligeuza eneo la Jangwani kuwa bustani kubwa ya jiji ambayo itapandwa aina kadhaa za miti adimu, huku mto Msimbazi ukipanuliwa kama ule mfereji mpana wa jijini Mwanza.

“Sina hakika zaidi kuhusu ule mfereji wa Mwanza, lakini nadhani ulijengwa enzi ya ukoloni maana kila mafuriko yanapotokea milima ya Mabatini hupita humo kiasi cha kupunguza maafa ambayo yangetokea katikati ya jiji la Mwanza,” amesema Zorro.

“Tujenge kama City Park ya New York au Bays Water London ambapo nina hakika wakati wa kiangazi itazalisha kipato kwa jiji. Tuweke Wanyama wadogowadogo humo kama vile swala pamoja na burudani za kifamilia,” ameongeza mkongwe huyo.


“Tokea nimezaliwa Mwanza yamepita mafuriko kama manne lakini madhara hayakuwa makubwa sana. Lakini kwa hapa Dar es Salaam, tangu nipo mdogo, kipande cha barabara kutokea Faya mpaka Mapipa au Shibam huwa na matengenezo kila miaka mitano au sita!”

No comments